Simulizi za ALLY H.

Simulizi za ALLY H.

Share

Huu ni uwanja unahusu simulizi za maisha zenye kuburudisha na kuelimisha lakini zenye kuzingatia maa

07/04/2025

SIMULIZI: SECRET
MUANDISHI: ALLY H.
Cont: 0677861890

SEHEMU 05

Upepo uliotokea baharini ulileta harufu ya chumvi na maua, na sauti ya muziki wa taarab uliokuwa ukipigwa taratibu kutoka kona ya mgahawa uliongeza mvuto wa mazingira.

Ndani ya mgahawa huo wa kifahari, macho ya Ibra yalimnasa Dabrina mara moja. Alikuwa nyuma ya kaunta ya vinywaji, akihudumia wateja kwa ustadi wa kazi aliyoiweza. Lakini alipoona sura ya mwanamke huyo mrembo, kila kitu kilisimama kwa sekunde chache.

Kulikuwa na huzuni iliyojificha nyuma ya macho yake ya kahawia, lakini bado tabasamu lake lilikuwa na joto la kuweza kuyeyusha barafu.

Ibra alichukua menyu na kujipeleka moja kwa moja mezani alipokaa Dabrina.

“Habari za jioni!". Ibra alisema kwa sauti yenye utulivu lakini iliyokuwa na chembe ya ucheshi.

"Nzuri habari yako nawe!". Kwa upole Dabrina alijibu.

“Habari ni njema kabisa, kwa jina naitwa Ibra, kwa huduma nzuri na ucheshi wa bure karibu sana.”

Dabrina alicheka kidogo. “Asante Ibra. Mimi naitwa Dabrina.”

“Jina zuri sana,” Ibra alijibu huku akiinamisha kichwa kwa heshima. “Karibu Zanzibar, Dabrina.”

"Asante sana!". Dabrina alijibu kisha akatulia na kumtupia jicho muhudumu huyo aliyesimama mbele yake.

“Naomba nikukaribishe kwa mara nyengine kwenye mgahawa wetu kwa chakula kitamu zaidi visiwani Zanzibar. Hapa tunahakikisha huondoki bila tumbo lako kushukuru.”

Dabrina alitabasamu kidogo, lakini hakutaka kuonekana k**a alikuwa akivutiwa. “Sawa, hebu nione kwenye menyu,” alisema huku akichukua orodha ya chakula.

Ibra alitabasamu na kuinamisha kichwa kidogo. “Ningependekeza uanze na supu yetu ya n**i na kamba, inasemekana ikigusa ulimi, unajikuta unarudi hapa kila siku.”

Dabrina alimtazama kwa macho ya kutilia shaka, “Una hakika?”

Ibra alitikisa kichwa. “Mimi siwezi kudanganya mteja mzuri k**a wewe. Na k**a haitakuwa tamu, nitakulipia chakula chote usiku wa leo.”

Dabrina alitikisa kichwa kwa tabasamu dogo. “Sawa, nitakula hiyo. Halafu nataka samaki wa kupaka na wali wa n**i.”

Ibra alipiga makofi kimzaha. “Umechagua sahihi! Chakula hiki kilichangia ndoa nyingi visiwani Zanzibar hasa wali wa n**i, ukisikia harufu yake tu, moyo wako unayeyuka!”

Dabrina alicheka kidogo. Hakuamini k**a mhudumu angeweza kuwa na ucheshi kiasi hicho.

“Na kwa vinywaji?” Ibra aliuliza.

“Juisi ya nanasi,” alijibu..

Muda haukupita, chakula chake kililetwa. Harufu nzuri ya n**i na viungo vya Zanzibar ilijaza hewa, na Dabrina alihisi furaha isiyoelezeka alipouonja ule wali.

“Mmmh… ni kweli, chakula hiki kina mvuto wa ajabu,” alisema huku akimtazama Ibra kwa jicho la pili.

Ibra alitikisa kichwa kwa tabasamu. “Nilikwambia, ukiondoka hapa kesho, moyo wako utabaki kwenye hii hoteli.”

Dabrina hakusema chochote, lakini kwa namna fulani, alihisi k**a maneno ya Ibra yalikuwa na maana zaidi ya chakula.

Baada ya chakula, alikaa kwa muda akitazama mawimbi ya bahari kupitia dirisha kubwa la mgahawa. Miale ya jua iliyokuwa ikizama baharini ilitengeneza mandhari ya kupendeza, k**a picha ya tumaini iliyochorwa juu ya huzuni yake. Kulikuwa na hali ya utulivu ambayo aliihitaji sana usiku huo.

***********************************
Asubuhi ilipofika, anga lilikuwa na mawingu mepesi na upepo wa bahari ulikuwa bado wa upole. Dabrina aliamka mapema, akajifungasha kwa ajili safari.

Alilipa bili yake mapokezi, akavua hereni zake kubwa na kuzihifadhi, kana kwamba alitaka kusahau kila kitu kilichompendezesha usiku uliopita. Mapema sana alowahi bandarini kuchukua boti ya mapema kuelekea Tanga, akiwa na mzigo mmoja wa nguo lakini mzigo mkubwa zaidi ulikuwa moyoni mwake.

Asubuhi hiyo ilikuwa tofauti kwa Ibra. Alipoamka, alijikuta akifanya maandalizi ya kwenda kazini kwa haraka lakini kwa hisia mpya ambazo hakuwa nazo siku zilizopita.

Alitembea kuelekea hotelini huku moyo wake ukiwa na shauku isiyoelezeka. Kila hatua ilimbeba kwenye matarajio ya kumuona tena mrembo yule aliyempokea jana usiku. "Dabrina" alijiambia kimoyomoyo, jina lake likiingia kwenye fikra zake k**a wimbo wa taratibu wa baharini.

“Hakika, ni mwanamke mzuri kuwahi kutokea mbele ya macho yangu,” alijiwazia.

Alipofika hotelini, alikutana na taarifa ambayo hakuitarajia. Dabrina alikuwa ameshaondoka.

Moja kwa moja, alielekea sehemu ya mapokezi ya wageni. Akapitia orodha ya wageni kuona k**a angebahatika walau kupata mawasiliano lakini kwa bahati mbaya juhudi zake ziligonga mwamba, aliziona namba za Dabrina lakini kulikosekana tarakimu moja, namba za simu alizotafuta hazikutimia zilikuwa tisa tu. Inaonekana aliandika kwa haraka, au labda kwa kuchanganyikiwa wakati wa kujaza fomu alisahau kumalizia.

Ibra alisimama pale kwa muda, akinyamaza huku macho yake yakikodolea jina lake tu.

"Namba haijakamilika..." alijisemea kwa sauti ya chini, k**a akizungumza na hewa. Akaweka daftari chini kwa upole, k**a vile lina mabaki ya mtu aliyekuwa muhimu.

Alijikuta akienda kukaa kwenye meza ile ile ambayo Dabrina alikalia. Alijishika kichwani kwa mkono mmoja, akihema taratibu. Hakujua kwa nini alihisi pengo hilo kubwa. Alijilaumu, "Kwa nini sikuuliza namba yake? Kwa nini niliruhusu aondoke bila kusema lolote?"

Kulikuwa na huzuni isiyoelezeka machoni pake. Mgongoni mwake palijaa uzito wa jambo ambalo hakuwa nalo tena nafasi iliyompita, kimya kilichomuuma zaidi kwa sababu hakikutoa nafasi ya pili.

"Nitamwona tena?". Alijiuliza bila kuwa na jibu sahihi.

****************************

Upande wa pili, Dabrina alikuwa ameketi karibu na dirisha la boti ya kisasa iliyokuwa ikielekea Tanga. Wakati huo bahari iling’aa kwa miale ya jua la asubuhi.

Dabrina alikuwa kimya, lakini ndani ya moyo wake kulikuwa na tafakari nyingi. Alijisikia vizuri kwa namna alivyopokelewa Zanzibar. Huduma ya hoteli ilikuwa ya kuvutia, vyumba safi na vyenye harufu ya maua, chakula kitamu kilichojaa viungo vya pwani lakini zaidi ya yote, huduma ya mhudumu mmoja wa mgahawa ambaye hakumsahau hata baada ya kuondoka.

Aliukumbuka ucheshi wa Ibra vile alivyomwelezea supu ya kamba na n**i, ahadi yake ya kulipia chakula endapo hakingekuwa kitamu, na maneno yake ya mwisho kuhusu juisi ya limau kusababisha ndoto za ajabu.

Alitabasamu mwenyewe, halafu akatikisa kichwa.

“Yule mhudumu alikuwa na ucheshi wa ajabu... sijui kwa nini? ananikumbusha namna mtu anatakiwa kuwa na utu, hata kwa wageni,” alijiambia kimoyomoyo.

Alihisi furaha ya ndani, si kwa sababu ya Ibra tu, bali kwa sababu kwa mara ya kwanza katika siku nyingi, alihisi kuguswa na utu wa mtu asiyejua chochote kuhusu maumivu yake ya moyo.

Alikumbatia mkoba wake kifuani, akajiinamia, akitazama bahari nje ya dirisha. Safari ya kurudi Tanga haikumaanisha tu kurudi nyumbani ilimaanisha pia kuondoka sehemu iliyomgusa kidogo zaidi ya alivyojiandaa.

Lakini moyoni, alikuwa na hisia kwamba siku moja, k**a bahari haikumsahau, basi huenda atarudi tena Zanzibar.........

ITAENDELEA.......
USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA........

06/04/2025

Habari! Ndgu wafatiliaji wote wa simulizi, ukurasa huu ulipoa kabisa kwa mda mrefu lakini sasa hautapoa, nimerejea na simulizi ya secret ambayo itawekwa hapa kila siku. Lakini muda huo huo inaandaliwa nyengine ambayo itakuwa inaruka pamoja. Ninaomba ushirikiano wenu tafadhali.🙏

06/04/2025

SIMULIZI: SECRET
MUANDISHI: ALLY H.
Cont: 0677861890

SEHEMU YA 04
*Dodoma*
Asubuhi ya Jumamosi, jua la Dodoma lilikuwa na mwanga mkali, lakini kwa Dabrina, dunia ilikuwa ya kijivu. Alijipamba kwa gauni lenye rangi tofauti tofauti lililomkaa vyema. Alikuwa akielekea kwa Yadash, mpenzi wake. Alitamani kupumzika kifuani mwake, kula kifungua kinywa cha pamoja, na kupangilia wikendi yao kwa bashasha. Siku hiyo aliamua kupendeza kuliko kawaida kwa ajili ya kuzidi kumvutia mpenzi wake lakini pia aliamua kumnunulia saa nzuri ya bei mbaya, ambayo aliihifadhi kwenye mkoba wake. Hakumpa taarifa aliamua kumsuprise kwani alitambua fika kwa muda huo lazima angemkuta.

Hakika Dabrina, hakujua ubaya wa siku hiyo, ni k**a hakutakiwa kwenda kwa mpenzi wake kwa kile kilichoenda kumkuta.

Alipofika mlangoni, aliukuta mlango umeegeshwa tu. Hakugonga aliusukuma kwa upole, akidhani atamkuta Yadash amelala au akisoma. Lakini alipofungua mlango, aliganda.

Picha aliyokumbana nayo ilimvuruga akili.

Yadash alikuwa ameketi kwenye kochi, kifua wazi, akiwa amejibweteka k**a aliyechoka baada ya tendo zito. Kando yake alikuwapo Grace, rafiki wa karibu wa Dabrina akiwa amejifunika kwa kitenge kidogo, nywele zake zikiwa bado hazijakaa sawa, shingo yake ikiwa na alama nyekundu za busu.

Sekunde zilisimama. Mapigo ya moyo wa Dabrina yakapoteza mpangilio.

“Hivi… nini kinaendelea hapa?!” sauti yake ilipasuka kwa mchanganyiko wa hasira na maumivu, ikitikisa sebule nzima.

Yadash aligeuka, akitabasamu kwa kutojali, kana kwamba hakuwa amefanya kosa lolote. “Dabrina… si tulikubaliana kuwa ukija, unanipa taarifa?” alisema kwa sauti laini lakini ya dharau.

“Unanitania?, kumbe nikikupa taarifa ndio unapata nafasi ya kuficha uchafu wako?” Dabrina alipaza sauti. “Hivi hii ni ndoto au ni kweli macho yangu yanaona hivi?! Rafiki yangu mwenyewe… Grace?!”

Grace alijikunja kwenye kochi, lakini uso wake haukuonyesha aibu. Alitabasamu taratibu, akamwangalia Dabrina kwa jicho la kejeli. “Pole dada… mapenzi hayana huruma.”

“Grace!” Dabrina aling’aka, akimwelekea. “Umenikosea heshima! Umenidhalilisha! Tulikula, tulilala pamoja... na leo hii unanifanyia hivi?!”

Grace alisimama, akajirekebisha kitenge chake, kisha akasema kwa ukali, “Usinielekezee vidole vyako. K**a hufai kwake, hufai tu. Uwepo wangu kwake haufuti chochote ila umechelewa kufumbuka macho, mimi na Yadash tupo kitambo, nakushangaa wewe king'ang'anizi.”

Dabrina alitikisa kichwa kwa maumivu. Machozi yalikuwa tayari yanachuruzika mashavuni. “Yadash… huoni haya? Hivi kweli... baada ya yote tuliyopitia?”

Yadash alikuna kidevu chake kwa utulivu wa ajabu. “Dabrina, ni heri ungefuata njia uliyojia, kila kitu umeshakifahamu tayari, siwezi kuishi wewe mtu wa drama na makelele ya kila siku.”

“Drama?!” Dabrina alipiga kelele. “Unaiita hii drama?! Moyo wangu uliokupenda unaitwa kelele?!”

“Naona huelewi tu,” Yadash alisema kwa sauti ya kutojali. “Nilishachoka muda. Grace ananielewa. Hana matatizo k**a wewe. Kitu kikiisha, kinaisha. Na... kwa taarifa yako” akamsogelea karibu Dabrina na kusema kwa sauti ya matusi “hata hukuwahi kunitosheleza.”

Dabrina alinyamaza. Maneno hayo yalikuwa risasi ya mwisho. Alianguka sakafuni kwa magoti, akilia kwa uchungu usioelezeka. “Nilikupenda… kwa moyo wangu wote.”

Yadash aligeuka kwa tabasamu la ushindi, akamshika Grace kiuno na kisha kumbusu mdomoni. Kwa pamoja walimgeukia Dabrina na kumtazama kwa macho ya dhihaka. Tukio hilo lilikuwa k**a msumari wa moto uliokandamizwa kwenye moyo wa Dabrina. Alijisikia maumivu makali sana ambayo hajawahi kuyasikia tangu aingie kwenye ulimwengu huu.

Bila kupoteza muda Dabrina alijizoa zoa pale sakafuni alipokuwa na kusimama taratibu, macho yake yalikuwa mekundu. Akakaza meno, akajifuta machozi kwa kiganja.

“Nawaachia kila kitu, uhusiano, na urafiki. Ila kumbukeni... kilichoanza kwa usaliti, hakiwezi kustawi.”

Akatoka. Mlango alifunga kwa nguvu kiasi kwamba ukuta ulitetemeka. Nje, alikimbia bila kuangalia nyuma. Kila hatua ilikuwa k**a kisu kinachochoma moyo wake. Alilia... si kwa sababu ya kupoteza, bali kwa kuamini kupita kiasi.

Alijikuta amefika kwenye bustani ya karibu na chuo, ile waliyoizoea kukaa na Yadash wakati wa mchana kujadili maisha yao ya baadaye. Viti vilikuwa vitupu, maua yakining’inia kwa upepo hafifu, kila kitu kilionekana kimya.

Alijikunyata kwenye moja ya benchi, akautoa mkoba wake na kuifungua ile sanduku ndogo iliyokuwa na saa aliyomnunulia Yadash. Aliitazama kwa sekunde kadhaa. Saa hiyo ilikuwa ya dhahabu laini, na maandishi madogo ya "To my love-Always yours".

Aliitazama kwa macho yaliyolowa, kisha akatabasamu kwa huzuni. “Kwa upendo wangu... kweli nimeishia hivi?” alijiuliza kwa sauti ya kuishiwa.

Akaiviringisha ile sanduku kwa hasira, ikapaa hewani na kudondoka kwenye nyasi. Aliinama kuichukua, lakini alikosa nguvu. Mikono yake ilitetemeka. Akakumbatia magoti yake, akaangua kilio kilichotoka rohoni.

Watu waliokuwa wakipita pembeni ya bustani walimkodolea macho kwa mshangao, lakini hakuna aliyeweza kufikia maumivu aliyokuwa anayapitia. Ilikuwa ni k**a dunia imemgeuka ghafla, na moyo wake ulipasuliwa vipande vipande bila huruma.

Dakika ziligeuka kuwa saa. Hatimaye, alisimama kwa tabu, akaanza kutembea polepole kuelekea nyumbani kwake. Kila hatua ikiongeza uzito wa uchovu aliouvaa moyoni. Nyumba ya kupanga aliyokuwa akiishi ilipomkaribia alifungua mlango, akaingia chumbani bila hata kuvua viatu, na kujirusha kitandani akiwa na nguo zake zote.

Alijifunika shuka lote, giza likamkumbatia k**a mfariji wa mwisho. Alitamani dunia isimame. Alitamani asiamke kesho.

Lakini moyo wake ulikuwa bado unapiga, ukiugulia, ukihema, ukilia kimyakimya.

Alijua atapona, lakini si leo. Si kesho. Labda si hata wiki ijayo. Maumivu yalikuwa yamejenga kambi, na kulikuwa na safari ndefu ya kuyaondoa.

Siku kadhaa zilipita japo kwa taabu sana, Dabrina alikuwa na wakati mgumu kuliko kawaida.

Likizo ikawa imewadia, na Dabrina aliamua kurudi kwao Tanga. Alijua kuwa nyumbani kungekuwa mahali salama kwake baada ya huzuni aliyokuwa akipitia. Hata hivyo, moyo wake haukuwa na haraka ya kurudi moja kwa moja. Alitaka sehemu ya kupumzika, kutuliza akili yake na pengine kusahau kidogo yaliyompata.

Ndipo wazo la Zanzibar lilipomjia. Kisiwa hicho kilikuwa na sifa ya utulivu, mazingira mazuri na fukwe za kuvutia. Bila kufikiria mara mbili, aliamua aelekee huko walau siku mbili kabla ya kurejea nyumbani.

****ZANZIBAR*******

Dabrina aliwasili jioni sana, upepo mwanana wa bahari ulimkaribisha kwa utulivu. Aliingia katika hoteli moja ya kifahari iliyo kando ya bahari, hoteli ambayo ilijulikana kwa mandhari yake ya kupendeza na huduma bora kwa wageni.

Ukumbi wa mapokezi ulikuwa umetengenezwa kwa mbao za asili zenye nakshi za Kizanzibari, na taa zilizotundikwa juu zilitengeneza mwanga wa kuvutia. Harufu ya maua ya jasmini ilienea hewani, ikiipa hoteli hiyo hisia ya ukaribisho wa kipekee.

Dabrina alipewa chumba chenye mandhari ya bahari, na alipolala kwenye kitanda chake cha kifahari usiku ule wa kwanza, alihisi k**a ameingia katika ulimwengu tofauti ulimwengu usio na huzuni wala msongo wa mawazo.

Hatimae ikawa siku ya pili, baada ya siku nzima ya kupumzika na kutembea kando ya fukwe, nyakati za jioni aliamua kwenda mgahawani kupata chakula cha usiku ndani ya hiyo Hoteli.

Akiwa amevalia gauni refu jeupe lililombana kwa ustadi, nywele zake zikiwa zimeachwa huru mabegani, alishuka taratibu kwenye ngazi kuelekea mgahawani. Sakafu ya marumaru ilitoa mwangaza hafifu, ikichanganyika na sauti ya mawimbi ya bahari yaliyokuwa karibu.

Ndani ya mgahawa huo wa kifahari, kulikuwa na viti vya mbao vyenye nakshi vikiwa vimepangwa kwa ustadi, na kila meza ilipambwa kwa mishumaa midogo iliyotoa mwanga wa kuvutia.

Ibra alikuwa nyuma ya kaunta ya vinywaji wakati alipomwona mgeni huyo. Kwa muda mfupi, moyo wake ulipiga kwa kasi. Uzuri wa mwanamke huyo haukuwa wa kawaida. Alikuwa na haiba ya kipekee, mchanganyiko wa utulivu na mvuto wa ajabu. Hakuwa mwengine, alikuwa ni Dabrina ambae alikuwa akitazamwa na macho ya Ibra.

Ibra hakuwa na shaka alijua ni mgeni kwenye hoteli hiyo. Alimtazama kwa sekunde chache kabla ya kuelekea kwenye meza yake huku akishikilia orodha ya vyakula .......................

Itaendelea............

*Naam sasa, Dabrina ameangukia katika Hoteli anayofanyia kazi Ibra.. unadhani kuna jambo litatokea baada ya hawa watu kukutana hapo?, usijipe mzigo wa maswali, subiria SEHEMU inayofuata...*

Nakusihi usikose sehemu inayofuata ya mkasa huu.

05/04/2025

SIMULIZI: SECRET
MUANDISHI: ALLY H.

SEHEMU YA 03

*Dar es salaam*
Ibra alifika kwa haraka kwenye mitaa ya Maputo, akijua kuwa kile alichokuwa akifanya kilikuwa cha dharura. Alkuta mlango wa chumba cha flora ukiwa haujafungwa vizuri. Aliusukuma na moja kwa moja akaingia ndani, macho yake yakagongana na taswira ya kusikitisha, Flora alikuwa amelala sakafuni akiwa amejikunja huku akipumua kwa shida. Maumivu yalikuwa wazi usoni mwake, macho yake yakionyesha uhitaji wa msaada wa haraka.

"Flora!" Ibra alipiga kelele kwa hofu na kumkimbilia. "Mungu wangu... Flora, unasikia sauti yangu?"

Flora alijaribu kuinua mkono lakini akaishiwa nguvu. Ibra hakupoteza muda. Alitoka mbio na kuanza kuomba msaada kwa watu waliokuwa jirani. Wawili kati yao walijitokeza haraka, na kwa pamoja walimwinua Flora kwa tahadhari na kumkimbiza hospitali iliyo karibu.

Hospitalini, wauguzi walichukua hatua za haraka. Ibra, akiwa na macho mekundu kwa wasiwasi, alielekea kwa daktari wa zamu na kuelezea kila kitu kwa haraka.

“Tutamuweka chini ya uangalizi wa karibu,” daktari alimhakikishia. “Anaweza kuwa na matatizo ya mfumo wa upumuaji, lakini tutaangalia kwa kina.”

Ibra alikaa hospitalini usiku kucha, akitazama dari, akifunga macho lakini mawazo yakiwa mbali. Alijua Flora hakuwa na ndugu yeyote jijini. Ilikuwa ni yeye peke yake sasa.

Siku tatu zilipita. Flora alianza kuimarika. Ingawa sauti yake ilikuwa dhaifu na mwili wake ilikuwa umechoka, macho yake yalikuwa na nuru mpya.

“Flora...” aliongea kwa sauti ya unyonge, “asante kwa kila kitu... sijui ningekuwa wapi k**a usingekuwepo.”

Ibra alimshika mkono, akasita sekunde chache kabla ya kujibu. “Usifikirie hilo sasa. Muhimu ni kwamba uko hai, shukrani kubwa ni kwa Mungu tu!”

Walitazamana kwa kimya, kila mmoja akiwa na maneno ambayo hakuyasema. Walikuwa watu wawili waliotoka katika maisha tofauti, walikutana katika vile viwanja ambavyo kina dada huuza miili yao, Ibra alibahatika kuwa mteja wa Flora.

Siku ya nne, daktari alitoa ruhusa ya Flora kurudi nyumbani. Ibra alikuwepo mapema, alimchukua na pikipiki yake mpaka katika nyumba aliyokuwa akiishi. Chumba chake kilikuwa kidogo ambacho kilitoa harufu ya kahawa na sabuni ya mche.

Flora alikaa kitandani taratibu, kisha akatazama mzunguko wa chumba kwa tabasamu dogo. “Ni mahali pazuri... kwa mtu mwenye moyo mzuri k**a wako.”

Ibra alitaka kujibu, lakini kabla hajafungua mdomo, simu yake ililia. Aliinyanyua mezani, akitarajia huenda ni wateja wake wa bodaboda. Alipoona jina la anayepiga, alishtuka kidogo. Mpigaji wa simu hiyo mara nyingi hutoa taarifa za kuhuzunisha, hakuwa na uhakika k**a simu hiyo ilikuwa na usalama.

'Mjomba Masudi'. Jina lilisomeka hivo.

Aliipokea kwa sauti ya kawaida. “Shikamoo mjomba.”

Kulikuwa na ukimya mfupi kabla ya sauti nzito yenye huzuni kuja upande wa pili.

“Ibra... naomba ukubali kuwa imetokea.”

“Imetokea nini, mjomba?” Ibra aliuliza kwa sauti ya mshangao.

“Baba yako... mzee wetu, amefariki leo alfajiri. Msiba uko nyumbani hapa.”

K**a mtu aliepigwa na radi, Ibra alishika kichwa chake, macho yalimtoka, ulimi ukawa mzito. “Unasema nini, mjomba? Hapana... baba? Hapana…”

Flora alimtazama Ibra kwa hofu, akisimama kwa taabu. “Ibra? Kuna nini?”

Ibra hakuweza kujibu. Alinyamaza kwa muda, kisha akatazama chini kwa macho yaliyojaa machozi yaliyogoma kumwagika.

“Baba yangu... hatarudi tena,” alijibu kwa sauti ya kukata tamaa.

Flora alimsogelea, akamkumbatia taratibu, kimya kikatawala chumba kizima. Hakukuwa na maneno sahihi ya kusema, lakini mguso wa mtu aliyekuwepo ulikuwa tiba ya muda mfupi.

Bila kupoteza muda Ibra alianza kujiandaa kwa safari ya kwenda Zanzibar. Kichwani mwake kulikuwa na mvua ya mawazo, maumivu ya kumpoteza baba, hatima ya maisha yake, na mkanganyiko wa hisia alizokuwa nazo kwa Flora. Haikuchukua muda Ibra alikuwa tayari kwa safari. Alimsihi Flora abakie hapo mpaka ataporejea baada ya Mazishi, hilo halikuwa na kipingamizi kwake.

Flora hakutaka kumuacha Ibra pekeake aliamua kumsindikiza mpaka bandarini. Kabla hajapanda meli, alimsogelea na kusema kwa sauti ya upole, “Ukiwa huko, kumbuka haupo peke yako. Nipo hapa, nikikusubiri.”

Ibra alimtazama Frola kwa macho mazito. “Naamini hatima ya maisha yetu huandikwa kwa njia zisizotarajiwa. asante kwa kila kitu, Flora.”

Kisha akaingia kwenye meli, huku upepo wa bahari uliochanganyika na chumvi ukivuma kwa shangwe.

Safari ya kwenda Zanzibar haikuwa nyepesi kwa Ibra. Kila upepo uliogusa ngozi yake ulikuwa k**a kumbukumbu ya baba yake aliyetangulia. Alipofika kisiwani, alipokewa na radi ya vilio na simanzi. Nyumbani kwao kulikuwa na kimya cha majonzi. Aliwakuta ndugu wakiwa wamekaa katika duara, kila mmoja akiwa na macho mekundu.

Lakini hakukuwa na kitu kilichomgusa k**a kumuona mama yake akiwa amekaa peke yake pembezoni mwa banda, akiwa ameshikilia khanga ya bluu aliyokuwa ameivaa mara ya mwisho walipoongea. Macho yake yalikuwa hayana nuru, yamejaa uchovu na huzuni isiyo na kifani.

"Mama..." Ibra alimsogelea taratibu, sauti yake ikivunjika.

Mama yake alimtazama, machozi yakimtiririka kimya kimya. Hakusema kitu, bali alisimama na kumkumbatia kwa nguvu, kana kwamba angemvuta ndani ya moyo wake apate faraja.

Mazishi yalipita kwa majonzi makubwa. Ibra alishiriki kila hatua, kuanzia kuchimba kaburi hadi kumwaga mchanga wa mwisho. Kila punje ya udongo iliyoanguka juu ya kaburi ilikuwa k**a msumari kwenye moyo wake. Hakika ilikuwa ndo safari ya mwisho ya baba yake.

Baada ya siku chache za kukaa Zanzibar na kusaidia familia, Ibra aliamua kurudi Dar es Salaam ingawa kuna jambo lilikuwa likimchanganya sana, tangu walipoagana na Flora pale ferry hakuwahi kupokea simu kutoka kwake lakini pia kila alivyojaribu kumpigia Flora hakubahatika kumpata, Flora hakuwa hewani, jambo hili lilimkwaza sana Ibra, hakutaka kuliacha k**a lilivyo alijiapiza akikutana na Flora lazima amwambie kuwa huo sio ubinaadamu. Mbali na yote hayo, Ibra alitarajia angepokelewa kwa tabasamu na maneno ya faraja. Lakini kilichomkuta kilimvunja moyo kwa namna ambayo hakutarajia.

Alipofika kwenye chumba alichomwacha Flora, alikuta mlango umefungwa. Aligonga kwa nguvu, lakini hapakuwa na jibu. Mmiliki wa nyumba alipomuona, alimsogelea taratibu.

"Unamtafuta yule dada uliyekuwa nae hapa?" aliuliza kwa sauti ya pole.

"Ndio... Flora. Yuko wapi?" Ibra aliuliza kwa haraka.

"Aliondoka siku mbili zilizopita. Alisema anakwenda safari ya mbali. Aliondoka na mizigo yote, hakuacha hata karatasi."

Maneno hayo yalimpiga Ibra k**a upepo wa ghafla, hakimuingia akilini Flora aondoke na vitu vya chumbani kwake.

"Alisema anakwenda wapi?". Ibra aliuliza kwa shauku yenye hisia za hasira ndani yake.

Mzee alitikisa kichwa. "Hakutaja. Alisema tu asipoonekana, usijali, unataka kunambia hauna taarifa?" Mzee aliuliza kwa mshangao lakini Ibra hakujibu kitu.

Alikaa kwenye ngazi za chumba hicho kwa muda mrefu. Mawazo yalimjia kwa kasi, je, Flora alimkimbia? Au alilazimika kuondoka? Hakujua, na kutokujua huko kulimuumiza zaidi. Hisia za kuibwa vitu vyake zikatamalaki. Alianza kujiona k**a mtu asiye na akili kisawasawa, aliulaani mpaka moyo wake wa huruma. Ubinaadamu wake ulimlipa zaidi ya maumivu. Alijua amekosea sana kumuamini mwanamke yule.

Alizikusanya nguvu ili aanze kutafuta, alianzia kule alipokuwa akiishi Flora hakubahatika kumpata aliambiwa ameshahama. Kitandawili kikazidi kuwa kigumu katika namna ya kumpata. Baada ya siku kadhaa za kutafuta bila mafanikio, Ibra aliamua kuondoka Dar es Salaam. Moyo wake ulihitaji utulivu mpya. Akarejea Zanzibar, safari hii bila mwelekeo maalum, ila akiwa na kiu ya kuanza upya.

Kupitia kwa jamaa wa karibu, alipata kazi katika hoteli moja ya kitalii iliyopo pwani ya Nungwi. Hoteli hiyo ilikuwa tulivu, ikizungukwa na mitende na sauti ya mawimbi ya bahari. Ilikuwa sehemu nzuri ya kuficha maumivu ya moyo, angalau kwa muda.

Kila jioni alisimama ufukweni, akitazama maji ya bahari yakikumbatia mwamba, akijiuliza k**a Flora alikuwa salama na k**a angeweza kumuona tena. Lakini zaidi ya yote, alijua kuwa maisha lazima yaendelee, hata k**a vipande vyake vya moyoni vilikuwa havijakusanyika tena...

Itaendelea....
Nakusihi usiache kufatilia mkasa huu...

04/04/2025

SIMULIZI: SECRET
MUANDISHI: ALLY H.

SEHEMU YA 02

*DODOMA*
Ilikuwa ni majira ya saa tatu usiku ndani ya ukumbi mzuri uliopambwa kwa madoido ya aina yake. Nyimbo mbalimbali zilisikika kuhanikiza siku ya kuzaliwa ya msichana aitwae Dabrina. Kulikuwa na watu wengi ambao waliamua kuacha shughuli zao kwa ajili ya kushiriki tukio hilo la rafiki yao kipenzi. Hawa walikuwa ni wanafunzi wenzake ambao alikuwa akisoma nao, walio wengi walikuwa pair yani kila mmoja na mwenza wake.

"Sasa birthday girl tunakuhitaji usimame tafadhali, tukio linalofuata ni la kulishwa keki na mahbuba wako, sina shaka huyo ndo jamaa ambae ameushikilia moyo wako k**a mateka". M.C aliongea kwa mbwembwe na watu wote waliitika kwa shangwe huku wakipiga makofi.

Dabrina ni msichana mwenye maringo na dharau. Lakini siku hiyo alik**atika, alijikuta akipoteza hali ya kujiamini, aibu ilikuwa imemzonga. Hii ilitokana na kukosa uzoefu wa mambo hayo. Hata hafla yenyewe hakuitaka ispokuwa mpenzi wake ndie alieandaa kila kitu na kumsihi akubali kufanya sherehe hiyo. Bahati ilioje tukio lilifana na kuwa la aina yake.

Hatimae keki ilikatwa huku vigele gele vikisikika.
'Kata keki tulee! Kata keki tulee'.

"Haya sasa birthday girl anaenda kumlisha keki mwanaume mwenye bahati, kijana flani alievuruga akili ya mtoto mzuri atokae kuleee! mapenzi yalipo zaliwa, any way nisiseme sana tunahitaji keki hiyo mlishane kindegendege". M.C aliongea na kuufanya umati uamke kwa shangwe.

Dabrina alihisi mapigo ya moyo yakimwenda mbio, hakuwahi fanya kitu k**a hiko mbele ya hadhara lakini ilibidi afanye kwa kuogopa kujitia aibu. Taratibu alimgeugia mpenzi wake na kisha walilishana keki kwa mdomo huku watu wakiwapigia makofi.

Majira ya saa tano na nusu usiku sherehe iliisha na kila mmoja alishika njia yake. Dabrina na mpenzi wake waliamua kwenda kupumzika hotelini kwasababu party hiyo ilifanyika mwishoni mwa wiki, hakukuwa na ulazima wa kurudi chuoni.

************
Dabrina Omari Hassan, ni msichana mwenye umri wa Miaka 24. Ni mzaliwa wa Lushoto mkoani Tanga, ni mtoto wa mzee Omari Hassani na bi Najat Kassim. Mzee Omari ni meneja wa tawi la CRDB na bi Najat ni Mwalimu wa shule ya Sekondari.

Maisha yao si haba yalikuwa ni mazuri mno kwani walimudu kuwa na Nyumba nzuri na gari la kifahari. Si hivyo tu walikuwa na mashamba na vitega uchumi kadha wa kadha.

Wakati huo Dabrina alikuwa mwaka wa mwisho akimalizia kusomea shahada yake ya udaktari katika chuo kikuu cha Dodoma.

Dabrina ni miongoni mwa wasichana waliobahatika kupata maumbile mazuri kuanzia rangi, nywele, sura, mwili ulijengeka kiuanamke. Ni mrefu wa futi Tano na inch nne, hakuwa mnene wala mwembamba wa sifa. Kifupi Dabrina ni mwanamke ambae kila mwanaume angetamani kuwa nae.

Wahenga walisema kila kizuri hakikosi kasoro. Ni hivo hivo kwa Dabrina, yeye alikuwa na jeuri na dharau. Sifa hii ilimfanya kupunguza Idadi ya watu na wengine walimsema kuwa anajidai.

Upande wa mahusiano Dabrina hakuwa na tabia chafu ya kubadiri wanaume. Mwanaume wake alikuwa mmoja tu ambae aliitwa Yadash Malik. Kijana huyo ndie aliebahatika kuutoa usichana wake na mpaka muda huo walikuwa pamoja. Naam! huyo ndo Dabrina.

****************
Usiku ulikuwa na utulivu, upepo mwanana ulivuma kwa maringo, kana kwamba ulijua kuwa kuna moyo wa msichana aliyekuwa katika sintofahamu ya kimapenzi. Alikuwa kimya, si kwa hasira, si kwa huzuni, bali kwa wimbi la hisia alizoshindwa kuzielewa.

Walipofika hotelini, Yadash alimpokea kwa heshima, akamfungulia mlango wa chumba na kumpa mkono kwa staha.

"Nimefurahi sana kwa ajili yako leo," aliongea kwa sauti ya upole. Dabrina alitabasamu lakini hakujibu, moyo wake ukiwa na mashaka yaliyomjia ghafla. Alijiuliza, hivi huyu kweli ndiye mwanaume wa maisha yangu?

Usiku huo haukuwa wa kawaida. Dabrina alilala kitandani akiwa macho kwa muda mrefu. Alitazama dari kwa muda akiwaza mambo mengi, akili yake ikiwa na minong’ono ya ndani isiyoeleweka. Si kwamba alimchukia Yadash, la hasha. Alimpenda, lakini kulikuwa na kitu hakikukaa sawa. Alichukia jinsi kila kitu kilikuwa kinaenda kwa mpango wa Yadash bila yeye kujihusisha sana. Alitamani uhusiano wa usawa, wa kushirikishana ndoto na maamuzi, si uhusiano wa kushurutishwa kwa vitendo vya kifahari.

Asubuhi ilipofika, walirudi chuoni. Maisha yaliendelea k**a kawaida, mihadhara, vikao vya kujisomea, vicheko vya marafiki. Lakini katika yote hayo, moyo wa Dabrina ulianza kuwa na mshindo tofauti. Kulikuwa na ukimya uliovaa tabasamu, huzuni iliyojificha kwenye maringo yake ya kila siku.

Katika wiki zilizofuata, Dabrina alianza kuwa mpweke zaidi. Alijikuta akitafuta muda wa kukaa peke yake, kuandika mawazo yake kwenye daftari la siri, na mara nyingine kuandika mashairi yasiyo na jina. Marafiki waliona mabadiliko lakini hawakumwelewa. Waliamini labda ni presha ya mwaka wa mwisho chuoni.

Miezi michache baadaye, ratiba ya masomo ilipungua, na ndipo chuo kilipotangaza kuwa wanafunzi wangepata likizo ya wiki mbili kabla ya mitihani ya mwisho.

Ukarasa mpya wa hadithi ya Maisha ya Dabrina ulienda kufunguka..........

Itaendelea......
Nakusihi kufatilia mkasa huu mapenzi wa kusisimua.

04/04/2025

Ule uvumilivu nilioupanda katika jangwa lililofubaa kwa matumaini, eneo kame lisilo na rutuba, ulionekana k**a ndoto isiyo na uhalisia. Licha ya changamoto, jua kali lililowasha ardhi na upepo wa kukatisha tamaa, niliendelea kushikilia matumaini. Imani yangu ilikuwa k**a mbegu ndogo iliyopewa maji na subira, ikastawi polepole, hadi hatimaye nikavuna kile nilichopanda. Sasa, nimeshuhudia matunda ya kusubiri, nimepokea zawadi niliyostahili. Nashukuru!

Niliamini bila kuona, sikujua alipo wala hali yake, lakini moyo wangu ulimtafuta kwa maombi. Nilimuomba Mungu amjalie afya njema, amlinde na kumwandalia njia njema hadi siku aliyokusudiwa kuwa sehemu ya maisha yangu. Na sasa, hakika amefika. Amefika k**a majira yanavyobadilika, kwa utulivu na uhalisia wa kupendeza. Amefika yule ambaye moyo wangu ulikuwa ukimsubiri, yule ambaye nilikuwa nikiomba awe na sifa ninazopenda. Amefika, na moyo wangu unashuhudia kuwa subira ina malipo yake. Nashukuru!

Laiti ningepoteza uvumilivu, laiti ningekubali shinikizo la wakati, nisingetambua thamani ya kusubiri. Ningetupa hisia zangu kwa mtu ambaye hakuwa wangu, ningekuwa nimecheza na hatima yangu kwa kuridhika na kilicho mbele badala ya kungoja bora zaidi. Hakika aliyesema mvumilivu hula mbivu alizungumza kwa maarifa tele. Subira yavuta heri, na sasa nathibitisha. Ni kweli unaweza kuwa na kiu kiasi cha kukaribia kupoteza matumaini, lakini si sahihi kunywa sumu kwa sababu tu ya kiu hiyo. Subira! Subira ni zawadi ambayo huleta matokeo mazuri.

Na sasa, ninapoinua macho yangu na kumtazama, moyo wangu hujawa na furaha isiyo na kifani. Ni kana kwamba ulimwengu wote umesimama kushuhudia muujiza huu wa mapenzi. Ulimi hutamka neno "nakupenda" kwa wepesi, lakini mapigo ya moyo wangu husema zaidi ya hayo, yakihesabu kila pigo k**a saini ya hisia zangu kwake. Mwili wangu husisimka anapogusa ngozi yangu, joto la mikono yake laini likiniacha nikiwa na msukumo wa huba usio na kifani. Kila alicho nacho, kila tabasamu lake, kila sauti yake, ni sababu ya mimi kutabasamu pia.

Napenda vile anavyonitazama, namna macho yake yanavyoangaza kila anapotamka jina langu. Napenda jinsi anavyonifanya nihisi kuwa wa thamani, k**a nyota inayong'aa gizani. Sauti yake ni nyororo k**a wimbo mtulivu wa upepo wa jioni, na kila mara anapozungumza, nahisi kana kwamba moyo wangu unacheza na mawimbi ya bahari tulivu. Kila kukicha, ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi hii ya upendo wa kweli. Kwa mara ya kwanza, nahisi moyo wangu uko mahali unapostahili kuwa.

Hakika, uvumilivu ni mtihani, lakini matokeo yake ni k**a maua yanayochanua baada ya mvua ndefu. Na sasa, ninaposhuhudia haya yote, ninajua kuwa subira haikuwahi kuwa kazi bure. Nimepata kile nilichostahili. Nashukuru!

Want your business to be the top-listed Gym/sports Facility in Kilindoni?

Click here to claim your Sponsored Listing.

Location

Telephone

Website

Address

Kilindoni