Hadithi zetu

Hadithi zetu

Share

Hapa utapata Riwaya na Hadithi kali kutoka kwa Mwandishi, Mustafa Mtupa(Abainder)

09/06/2024

It was granted

23/09/2023

RIWAYA: MKWE WA RAIS
SEHEMU YA 02
MTUNZI: MUSTAFA MTUPA
MAWASILIANO: 0687 058 966
ILIPOISHIA
“Hee! Wewe unatokea wapi?”yule jamaa alionyesha kushangazwa baada ya Fred kuongea.
“Mimi naitwa Fred kaka natokea Tanzania,”alisema Fred kwa upole.
“Aaah, kumbe ndugu yangu kabisa, niambie, mimi natokea Kenya”yule jamaa aliongea huku akitabasamu.
Fred ikabidi amuelezee shida yake na jamaa hakuwa na hiyana alimpa simu ili atimize adhma yake.
ENDELEA

Fred alichukua simu haraka kwakuwa namba ya Mudi alishaiandika hadi kwenye karatasi haikuwa tabu sana aliiandika haraka kwenye simu na kuanza kuipiga kwa simu ya kawaida kwa kuwa yule Mkenya tayari alikuwa na laini ya Saudia.
Lakini alipokuwa akipiga haikupokelewa na mwisho ilizimwa, Fred aliishiwa pozi na alipoamua kumcheki Whatsapp bado Mudi hakuwa anapokea simu.
Fred alijikuta nguvu zinamuishia na akachuchumaa chini huku ameshika kichwa chake asijue hata nini afanye.
“Kaka vipi? Jamaa hajapokea au hapatikani”Yule Mkenya aliuliza.
“Ndugu yangu jamaa hapokei simu na mwisho amezima kabisa,”aliongea Fred na akashindwa kuendelea..akaangusha kilio.
“Sasa unalia nini kaka, mitihani tu ya kawaida hiyo, shukuru kwamba umekutana na mtu kutoka ukanda mmoja mnaongea lugha moja”alisema Yule Mkenya na kumnyanyua Fred.
“Mimi nahisi nina mikosi, nimepambana sana hadi kufikia hapa, lakini naona kupambana kwangu ni kazi bure,”Fred aliendelea kulalamika huku akilia.
“Wewe sikiliza ndugu yangu, k**a jamaa hapokei simu, hakuna shida usiwaze sana, twende ukalale nyumbani, mimi nipo hapa mwaka watano sasa nafanya kazi Hospitalini, nina sehemu ya kuishi utalala na kesho tutamatafuta tena, siwezi kukutupa hapa wewe ni ndugu yangu kabisa Mama yangu mimi ni Mtanzania”
Aliongea yule Mkenya na kumpa matumaini Fred aliyeonekana kuwa ameshakata tamaa.
Hata k**a ilikuwa ngumu kwa Fred kumuamini kirahisi jamaa yule, hakuwa na namna kwa sababu asingeweza kulala nje na aliona pengine Mungu amemtuma mtu huyo kwa ajili ya kumsaidia katika wakati huo mgumu.
“Mimi naitwa Thobias,”Yule Mkenya aliongea na kumpa mkono Fred ambaye aliupokea kisha naye akajitambulisha kwamba anaitwa Fred.
Baada ya hapo wakaongozana hadi nje ambapo walichukua taxi na kuanza safari ya kuelekea sehemu ambayo jamaa alikuwa akiishi.
Njiani Fred alikuwa akistaajabu ukubwa wa majengo mbali mbali na uzuri wa barabara ambazo zilikuwa zinapishana pishana, huku mataa yakiwa yanamulika sehemu zote, ilikuwa ni usiku wa manane lakini kutokana na mataa hayo palionekana ni k**a mchana.
Ilikuwa safari ya dakika 80 hadi kufikia sehemu ambayo ile taxi ilisimama na bila hata ya kuuliza bei Thobias alitoa pesa mfukoni mwake na kulipa, kisha akamwambia Fred washuke.
Kwenye nchi zilizoendelea taxi huwa zina kifaa maalumu kwenye eneo la kioo cha mbele, kifaa hicho huonyesha kilomita ambazo gari imetembea na kiasi unachotakiwa kulipa.
Baada ya kushuka kila mmoja alikokota mizigo yake na wakasogea kwenye moja ya jengo ambalo lilikuwa kimya sana.
Pembeni kidogo ya nyumba hiyo kulikuwa na supamaketi ambayo ilikuwa inauza matunda na bidhaa nyingine.
Wakati wameshuka kwenye ile teksi Fred alitupa macho yake kwenye mlango wa Supamaketi hiyo kwa muda kidogo akawa k**a mtu aliyekumbwa na butwaa.
Alimshuhudia mwanamke wa kizungu ambaye alikuwa na umri kati ya miaka 24 hadi 25, uzuri wa mwanamke huyo ndio ulisababisha Fred apigwe na butwaa akasahau hata k**a alikuwa kwenye hali ya sintofahamu kwenye nchi ya watu.
Mwanamke huyo alikuwa akitoka mlangoni huku pembeni akiwa na wanaume wawili ambao walikuwa wamevalia suti, miwani nyeusi na masikioni walikuwa na vifaa vilivyokuwa na waya zilizoingia kwenye makoti yao.
walikuwa na miiliki mikubwa iliyojazia na wao pia walikuwa ni wazungu na muda wote huwa huo walikuwa pembeni yake mwanamke huyo.
Baada ya kutoka nje tu.. tayari gari nyeusi iliyokuwa pembezoni mwa duka hilo likawa limefunguliwa mlango na yule dada akaingia.
Muda wote huo Fred alikuwa anashangaa hata akasahau kulisogeza begi alilokuwa amelishusha kutoka kwenye teksi iliyowafikia mahali hapo.
“Kaka unashangaa nini? Hii ndio Saudia, fata kilichokuleta.”Aliongea Thoby, huku akitabasamu akimuangalia Fred.
Maneno yale yalimfanya atoke kwenye bumbuwazi ambalo lilitokana na uzuri wa kiumbe alichokiona.
Dada huyo alikuwa na nywele za rangi ya Brown, macho ya bluu, mrefu na licha ya uzungu wake nyuma alikuwa amejazia kana kwamba ni mwanamke kibantu, hakuwa mnene wala mwembamba wa umbo.
Itatosha kumaliza riwaya nzima kusimulia jinsi Mungu alivyoweka neema zake juu yake na kumfanya aonekane k**a mmoja kati ya wanawake warembo kwa wale wanaomtazama.

Basi, baada ya mshangao na lile gari kuondoka, Fred akakokota begi lake kutoka kwenye teksi, kisha wakatembea hadi kwenye moja ya mlango na Thobias akabonyesha mahali kisha mlango huo ukafunguka na wakaingia, hiyo ilikuwa ni lifti ambayo iliwapandisha hadi kwenye ghorofa ya tano.
Wakaingia ndani, baada ya kuweka mizigo.. Thobias bila ya kumuuliza Fred aliisogea kwenye friji lililokuwepo ndani hapo na akatoka na mkate na juisi kisha akamwambia Fred kuwa anafahamu hakuwa amekula tangu afike hivyo apate chochote kitu.
Baada ya kumaliza kula Fred alijitupa kwenye kochi na kuanza kuutafuta usingizi ambao haukumchelewesha hata kwa dakika moja.
Kulala kwenye kochi kwa Fred ni kutaka mwenyewe kwani Thobias alimtaka akalale chumbani kisha yeye mwenyeji alale kwenye kochi, Fred alikataa kata kata na kusisitiza kwamba pale ukumbini kwenye kochi palikuwa panamtosha.
Usiku wa siku hiyo ukapita hivyo na kesho yake saa nne hivi asubuhi ndipo Fred aliamka akiwa na uchovu wa kutosha kutokana na mbilinge mbilinge za jana yake.
“Kaka vipi? Umeamka salama?”lilikuwa ni swali la kwanza la Thoby mara tu baada ya kutoka ukumbini na kumuona Fred akiwa tayari ameamka.
“Niko poa kaka namshukuru Mungu”alijibu Fred huku akiinamisha shingo yake upande wa kulia.
“K**a unachaji unaweza kunisaidia niipe moto simu yangu ili niongee na mwenyeji wangu”Aliongeza Fred na Thoby bila ya kutia neno alitembea hadi chumbani kwake na kutoka na chaja.
Haraka sana Fred aliichomeka simu yake na kuwasha ili kuanza kuperuzi na kumtafuta Mudi.
“Lakini hapa sina WIFI kwanini usitumie tu simu yangu?”wakati Fred akiiwasha simu yake Thoby akampa wazo ambalo lilionekana kuwa zuri Zaidi.
Aliipokea simu ya Thoby na kuanza kupiga tena namba ya Mudi lakini haikupolewa, akajaribu kuingia whatsapp ambako alimtumia ujumbe mfupi wa maandishi sambamba na ujumbe wa sauti(Voice note), lakini chakushangaza baada ya kutuma vitu hivyo, simu ilionyesha kwamba meseji zimesoma kwa sababu ilitokea vitiki viwili lakini hakukuwa na majibu.
Alijaribu kupiga pia kupitia Whatsapp lakini Thoby alimwambia kwamba kwenye nchi hiyo hapakuwa na Whatsapp call hivyo pengine Mudi anashindwa kupokea kwa kuwa hakuwa na VPN. Kwani ili kuongea na mtu ilikuwa lazima udownload VPN kwenye simu yako.
Simu ilionyesha kwamba Mudi anasoma meseji lakini hajibu, anasikilia voice note.. lakini hajibu.
Fred akachoka, mwili wake ukawa k**a umeloweshwa maji kutokana na hiko kilichokuwa kianendelea.
Aliona sasa rasmi rafiki yake huyo amemkataa na amemtupa kwenye nchi ya watu, nchi ambayo hakuwa na ndugu wala rafiki zaidi yake.
Uvumilivu wa kiume ulimshinda na akaachia kilio kwa sauti kubwa iliyosababisha Thoby aliyekuwa chumbani kwake anajiandaa kwa ajili ya kwenda kazini atoke haraka kwenda kutazama ni nini kimemkuta Fred.
“Kaka shida nini..mbona unalia sana?,’’aliuliza Thoby mara tu baada ya kufika ukumbini.
“Kaka maishaaa, maishaa kaka aaah!” aliongea Fred kwa msisitizio huku akishika kichwa chake kwa nguvu.
NINI KITATOKEA...?
ITAENDELEA
UNAWEZA KUIPATA FULL KUPITIA HAPA FACEBOOK AMA WHATSAPP KWA SHILINGI 5000, AU KIPANDE KIMOJA 500.

NICHEKI KUPITIA NAMBA 0687 058 966

21/09/2023

SEHEMU YA KWANZA

RIWAYA: MKWE WA RAIS
MTUNZI: MUSTAFA MTUPA
MAWASILIANO: 0687 058 966
“Wakinik**ata wataniua au wataninyonga tafadhali naomba unisaidie niondoke hapa kaka, nina familia inanitegemea, mimi ndio mtoto tegemeo nyumbani tafadhali nisaidie niondoke”
“Kiukweli kesi yako ni ngumu sana, sijui hata nakusaidia vipi ila ngoja tupambane tujue tunalimalizaje maana serikali ya nchi hii haina utani hata kidogo.”
…………Nini kimetokea? anza hapa…………

"NDIO hivyo bwana maisha yamekuwa magumu sana, lakini Mungu anasaidia tunapambana na mkono unaenda kinywani, hili ni jambo la kushukuru."
"Lakini umewaona wenzetu Abdul na Mudi.. wametoka nje na wamerudi mambo safi, mimi nawaza niongee nao wanipe mchongo, maana naona hapa ndani kila nikipambana naanguukia pua"
"Kwani jamaa wanafanya kazi gani kule..?"
"Nasikia wameenda kupika pika kwenye meli za mfuta lakini sina uhakika."
"Aah wewe bhana hata k**a anafanya deki lakini mpunga anaoupokea unaonekana mkubwa, tunachotafuta pesa tu, mimi mwanangu hata wakisema nikaoshe vyombo mimi naenda."
"Haya bhana mwanangu acha mimi nichomoke kuna mshikaji namuwahi hapo mbele, tutachekiana basi au vipi..”
Yalikuwa ni mazungumzo baina ya marafiki wawili waliokutana barabarani na kuamua kuyajadili magumu ya maisha wanayopita kabla ya kila mmoja wao kufikia adhimio la kuagana na kuahidiana kuwasiliana kupitia vifaa vyao vya mawasiliano.
Fredis Ibrahim Nakata ni kijana mwenye umri wa miaka 19, akiwa amemaliza kidato cha nne mwaka 2019, hakufanikiwa kuendelea mbele na badala yake aliamua kujishughulisha na biashara ndogo ndogo kwa ajili ya kuliendesha gurudumu la maisha.
Nyumbani kwao anaishi na mama yake sambamba na dada yake ambaye ana mtoto mmoja lakini baba wa mtoto alikataa ujauzito.
Baba yake Fred tayari alishafariki kabla hata yeye hajamaliza elimu yake ya sekondari, hivyo muda wote huo alikuwa akiishi na mama yake ambaye alikuwa akiuza maandazi kuhakikisha analisha familia yake na watoto wanaenda shule.
"Mwanangu, leo kaja hapa mwenye nyumba anataka kodi yake kabwaaata! hadi majirani wametoka nje nimejisikia aibu sana "
"Daah! hali yenyewe ngumu, si nilimwambia anivulimilie kidogo, kuna pesa natarajia kuipata ndani ya siku chache zijazo"Fred alijibu huku akishika kiuno.
"Sasa kauli hizo inabidi umwambie yeye ukikutana naye, ukiniambia mimi utakuwa unatwanga maji kwenye kinu, mimi k**a mwili wangu ungekuwa sawa ningekusaidia, lakini mwili huu ushakuwa mbovu nikitembe dakika 10 naanza kuhema k**a nimekimbizwa."

Yalikuwa ni mazungumzo ya mama Fred muda mfupi baada ya Fred kurudi nyumbani kutoka kwenye mihangaiko yake.

Mazungumzo hayo yaliendelea kwa muda kabla ya kupata chakula cha jioni na kila mmoja kushika njia ya kwenda kupumzisha mwili baada ya pilika pilika za mchana kutwa.
Usiku ulikucha, Fred alijiandaa asubuhi na mapema baada ya kupata kifungua kinywa alitoka kwenda sokoni kisha akarudi kwenye eneo lake la kufanyia kazi ambapo alikuwa amefungua genge dogo lenye nyanya, vitunguu na bidhaa nyingine.
Aliendelea kuuza uza licha ya kwamba biashara ilikuwa ngumu sana kwani kwa muonekano tu genge lake halikuwa na vitu vingi na watu wengi walikuwa wakimpita kwenda genge lililokuwa linapatikana hatua 20 kutoka alipokuwa yeye, genge hilo lilikuwa maarufu, watu walikuwa tayari kukaa foleni ili kupata huduma, wakati pale kwa Fred pakiwa patupu.
"Kijana kijana kijana……" Ilisikika sauti nzito gengeni kwa Fred na kwa uvivu akanyanyua sura yake kuangalia ni nani aliyekuwa anamwita.
Baada ya kunyanyua uso ambao haukuwa na chembe ya furaha hata ya kuongopa, ghafla Fred akaonekana kuuruhusu mdomo wake kufunguka na kutasabamu kwa kutoa meno nje kutokana na kile alichokiona.
"Heeee! Mudi..! ebanaaa eee kweli pesa haziongopi naona mwanangu unazidi kunenepa tu, kweli waarabu hawana kazi ndogo, umeenda miaka mitatu tu umerudi na shavu la kutosha"Aliongea Fred kwa mshangao.
"Acha kuzingua wewe, mimi mbona nipo kawaida, wewe ndio umefura k**a kifaru vile, naona chuma kimekukubali sana"Mudi naye akarudisha mapigo kwa kumpamba Fred.
"Aya bhana, wewe nicheke tu, mwili wa maandazi huu umekaa kaa tu, niambie mwanangu salama lakini? Tanzania umeingia lini?"
"Nimeingia juzi nilikuwa kwenye msiba Tanga, hapa nina siku tatu tu, itabidi nirudi tena Saudia, Nimepewa ruhusa ya muda mfupi kwa ajili ya msiba."
"Hee! nani kafariki?" aliuliza Fred.
"Nafikiri humjui, ni baba yangu mkubwa anakaa Tanga”

Fred na Mudi ni marafiki wa muda mrefu tangu utotoni, walisoma shule moja na walikuwa wakikaa mtaa mmoja kabla ya mudi kupata mchongo wa kwenda kufanya kazi nchini Saud Arabia kwenye moja ya migahawa.
Baada ya salamu na mazungumzo ya hapa na pale Mudi alimuaga Fred na kumwambia wangeonana baadae atakapokwenda gengeni kwake kupiga stori kwani muda huo alikuwa akihitaji kupumzika kutokana na uchovu wa safari.
Pesa kweli huwa haiongopi, Mudi aliondoka mtaani akiwa amekondeana na hana hata siha wala haiba lakini muonekano wake baada ya kukutana na Fred ulikuwa tofauti kabisa, alionekana kuwa mng'avu usoni hata mavazi aliyovaa yaliakisi ukwasi wa aina yake aliokuwa nao.
Baadaye kweli walikutana gengeni kwa Fred na kupiga stori mbili tatu wakikumbushiana baadhi ya mambo waliyowahi kufanya enzi zao za utoto.
Mwisho wa mazungumzo Fred aliitumia nafasi hiyo kumuomba Mudi ikiwa kuna nafasi huko yeye ambako anafanya, naye angetamani kwenda kufanya kwani maisha ya Tanzania yalikuwa yamemchosha na anafikiria kutoka huenda naye akabarikiwa.
"Aaah hilo mbona limeisha kaka, kwanza ni k**a umeniwahi tu, kiukweli kazi zipo, mimi nilipanga nije kukwambia tena mshahara ni mzuri tu, lakini kwanza lazima ufuatilie pasipoti alafu mambo mengine yatafuta, ila uhakika wa kazi upo. Kuna migahawa mingi inafatuta wafanyakazi." alisema Mudi.
"Aaah mwanangu nitashukuru sana, mimi hiyo pasipoti nitapambana niipate tu, maana nishachoka kukaa bongo, kila siku hali inazidi kuwa mbaya tu.'' aliongea Fred kwa sauti ya upole iliyoashiria uhitaji.
"Wewe usijali mwanangu, wewe ni rafiki yangu halafu mwanangu sana. Mimi nitakusaidia tu, kazi utapata kwa uwezo wa mungu."
Mudi alikaa Tanzania kwa siku kadhaa kisha akrejea tena Uarabuni kuendelea kuzitafuta pesa.
"Basi ndio k**a nilivyokwambia, hapo wewe kaa tayari na pasipoti yako, ili mimi mambo yakikaa sawa tu nakupa mchongo unapaa, hakuna kuremba tena hiyo," Mudi alikuwa akiongea huku akinyoosha nyoosha mikono kumwambia Fred ambaye kwa wakati huo alikuwa amemsindikiza uwanja wa ndege wakati anaondoka.
"Babu wewe hilo la pasipoti niachie mimi, yaani kesho tu mimi naanza mchakato wa kufuatilia, sitaki mchezo kabisa," aljibu Fred kwa msisitizo huku akipiga piga mikono yake.
Haikuchukua muda mrefu sana, Mudi alienda kukaguliwa na kupewa Boarding Pass tayari kwa ajili ya kuelekea sehemu ya kusubiria ndege ambayo ilimpeleka hadi Doha, Qatar kisha akabadilisha ndege iliyomfikisha Saud Arabia.
Siku mbili mbele kweli Fred alianza mchakato wa kufuatilia pasipoti ili kujiweka tayari muda wowote mchongo utakapotokea lakini changamoto kubwa kwake ilikuwa ni pesa.
Kawaida inamhitaji mtu kuwa na kiasi kisichopungua shilingi 200,000 kwa ajili ya kukamilisha mchakato wote, kwake ilikuwa ngumu kwani hali yake ya kimaisha ilikuwa mbaya sana.
"Nimekupigia tangu asubuhi jamani hupokei na nimekuja hadi gengeni sijakuona, shida nini kaisari wangu,"
"Aaah naumwa bhana, nimeamka kichwa kinanibangua sana, nipo tu nyumbani hata sokoni sijaenda."
"Jamani unaumwa na umeshindwa kuniambia yaani k**a tumegombana..hivi ni kweli Fred..?"
"Sio hivyo Ashura bhana, jana salio liliniishia usiku, hivyo leo tangu asubuhi sijatoka nje, ndio maana unaona sijakucheki malkia wangu"
"Aya mimi nakuja kukuona na najua tangu asubuhi haujala, nikuletee nini?"
"Wewe leta unachojisikia, mimi nitakula tu kwa sababu yako"
"Mwanaume una mbwembwe yeye, haya ngoja nije"
Huyo alikuwa ni Ashura, mpenzi wa Fred ambaye alianza kuwa kwenye uhusiano naye tangu wakiwa wanasoma elimu ya sekondari.
"Mama jamani hata mimi?" Ilikuwa ni neno la kwanza la Ashura mara baada ya kufika nyumbani kwa kina Fred na kumkuta mama yake akiosha vyombo.
"Nini tena mwanangu?"aliuliza Mama Fred huku akinawa mikono yake.
"Huyu Jambazi anaumwa tangu jana usiku, yeye hajaniambia nawewe mama hujaniambia."Aliongea Ashura huku akisogea karibu alipokuwa Mama Fred na mkononi akiwa ameshika mfuko mweusi.
"Mwanangu hiyo habari ya kuumwa ndio unaniambia wewe muda huu, mimi najua labda k**a kawaida yake kulala k**a samaki pono, sijuiii kabisaaa k**a anaumwa,"
"Nilikwambia mama humu mtoto huna si bora ungeenda kumbadilisha na gunia la mpunga Morogoro ukapata faida ya kula ubwabwa.''
"Hilo gunia la mpunga nalo kubwa nigewe tu maji ndoo moja namtoa mimi" Mama Fred na Aisha wamezoeana kwa muda mrefu na mbali yakuwa mtu na mka mwanawe walikuwa ni marafiki pia hivyo mara kwa mara wamekuwa wakitaniana na kubwa zaidi Mama Fred alikuwa ni Mndengeleko na Ashura ni Mmakonde, hivyo walikuwa na utani wa asili.
Baada ya mazungumzo ya muda mfupi Ashura aliingia chumbani kwa Fred.
"K**a unakuwa unataka kufa unatuambia tukuletee sanda kabisa usiwe unajikausha k**a hivi,"Mara baada tu ya kuingia ndani hiyo ndio ilikuwa kauli ya Ashura kumwambia mchumba wake Fred.
"Si nyie wamakonde mnanijaribu, jaribu subirieni zamu yangu ikifika nitampiga mtu kombola moja tu hatoamini."alijibu Fred na wote wakacheka.
Baada ya stori na hadhithi za hapa na pale Fred aliamka na kuanza kukishambulia chakula alicholetewa na baada ya muda mama yake pia alimletea dawa za kumeza ili kupunguza maumivu.
"Hicho kichwa nimekwambia siku nyingi ni kipanda uso, nenda kwa mama yako mkubwa akakuchanje hautaki. Utakula dawa kitapoa baada ya wiki kitauma tena, mtoto mbishi kweli wewe.''
''Basi mama nimekusikia nitaenda, acha kwanza hapa kipoe, maana hali ni mbaya"alijibu Fred na baada ya kula dawa na kupiga stori na Aisha kwa masaa kadhaa ikafikia wakati wa Aisha kuondoka, hivyo akamsindikiza hadi maeneo ya karibu na kwao kisha wakaagana.
"My nataka tuongee kitu, kesho k**a utakuwa na nafasi,"alisema Fred.
"Tufanye nikirudi kazini, nitakupigia tukutane, kwanza ni kitu gani,"Alijibu na Ashura na kuongeza swali.
"Acha mapepe wewe, subiri utakijua hiyo hiyo kesho.''
Ndege hao wawili walikaa ndani kwa pamoja kwa muda usiopungua masaa mawili na baadae Ashura alishika njia na kuondoka eneo hilo.
Mitaa ambayo Fred alikuwa akiishi ilikuwa ni Tabata, Kimanga ambapo pia Ashura alikuwa akiishi, ingawa utofauti ulikuwa ni kwamba Ashura aliishi Tabata, Mawezi na Fred aliishi Tabata Chama. Baada ya Ashura kuondoka Fred alirudi nyumbani na kuendelea kuuguza kichwa chake, mida ya jioni hivi baada ya kuona kimepoa akaamua kutoka nje kwenda kijiweni kupiga soga na vigano vya hapa na pale, pia kufungua biashara yake walau apate hata pesa ambayo itatumika kwa ajili ya vitafunio kesho yake asubuhi.
Kwa hakika Fred alikuwa kwenye kipindi cha mpito sana, ndoto yake kwa muda huo ilikuwa ni kutoboa kimaisha na hakuwa anaona uwezekano wa kufanikiwa kwa kuendelea kusalia nchini Tanzania kutokana na ugumu wa maisha ambao aliokuwa akikutana nao kwa wakati huo.
Licha ya kupambana katika kipindi chote hicho bado hakupata hata nusu ya kiasi cha pesa ambacho alitakiwa kuwa nacho kwa ajili ya kuanza mchakato wa maombi ya hati ya kusafiria.
Baada ya kufika kijiweni na kufungua biashara yake, kwa sababu ilikuwa ni jioni baadhi ya marafiki zake walienda kukaa kwenye benchi lililokuwa pembeni ya genge na kuanza kumwaga maneno.
“Mwanangu hapa nitampata nani nimuuzie hili genge anipe hata laki mbili..?”Fred alimuuliza mmoja ya marafiki zake waliokuwa kwenye benchi kwa muda huo aliyeitwa Rama.
“Hahahahaha, ndugu yangu unachekesha sana ”Rama akajibu swali la Fred kwa kicheko na kumsifia kwamba alikuwa akichekesha.
“Sasa rafiki yangu mimi nakuuliza jambo la msingi wewe unaniambia nachekesha, nachekesha nini sasa hapo”Fred alijibu na kuonyesha kuwa hakuwa amependezwa na kicheko cha Rama.
“Nacheka kwa sababu unanichekesha, sasa unavyoona hilo genge lako ambalo halina chochote nani atakuwa amepungua akili kiasi cha kukubali kutoa laki mbili kulinunua” Rama alijibu.
“Aaah hiyo kianzio, k**a hana laki mbili atashuka, atanipa hata laki.”
“Wewe sema unataka shingapi tujue moja, masuala ya kutumbia k**a hana laki mbili sijui mtashuka, mtapanda ni kupotezeana muda tu” Rama aliongezea baada ya Fred kuonekana hana uhakika juu ya kiasi gani hasa cha pesa anakihitaji ili kuuza genge lake.
“Basi tusiongee sana mambo yakawa mengi, wewe chekecha unavyojua, mimi nataka laki nianzie mchakato hiyo wa kufuatilia kitabu(Pasipoti), wewe k**a unamteja wa pesa hiyo mimi nachukua freshi,”alijibu Fred.
“Poa wewe nisikilizie, nitawashtua wadau kuanzia kesho… k**a nitapata mtu..nitakupa taarifa”Rama alijibu na kufunga mjadala huo mzito uliokuwa unaendelea.
Uzuri wa Rama ni kwamba alikuwa ni mmoja kati madalali wanaoaminika katika maeneo hayo, hivyo haikuwa ngumu sana yeye kutafuta wateja wanaoweza kutoa pesa kwa ajili ya genge hilo.
Baada ya kupita siku tatu mteja wa kununua genge alipatikana na akakubali kutoa shilingi laki moja.
Japokuwa haikuwa inatosha Fred hakuwa na jinsi Zaidi ya kukubali kwa sababu mwanzo wa mbili ni moja.
Bahati mbaya ni kwamba yeye ndio alikuwa akilisha pia familia hivyo kadri alivyokuwa anazidi kukaa nyumbani bila ya kazi ya kufanya ndivyo akawa anaichota ile aliyouzia genge kidogo kidogo.
Vilevile kiasi hicho cha pesa ilibidi pia kitumike kwenye kulipa kodi kwa sababu mwenye nyumba alikuwa akiwasumbua sana kwani walipitisha miezi minne bila ya kumlipa.
Hadi muda huo hakuwa amemwambia mama yake kwa sababu alikuwa akihofia kwamba huenda angetangaza halafu kwa ndugu zake wengine hivyo safari ingekuwa na gundu.
Siku ambayo aliweka ahadi ya kukutana na Aisha kwa ajili ya kumuambia suala hilo hawakufanikiwa kukutana..sababu ikiwa ni baada ya Aisha kupata msiba wa mmoja ya ndugu zake, hivyo walikutana baada ya wiki moja tangu wapeane ahadi.
“Unasemaaa? Haya unaenda kukaa kwa muda gani huko? Kwanza si ndio nasikia watu wanafanyiwa vitendo vibaya huko.. wanauliwa, wanatolewa mafigo wanateswa,”zilikuwa ni kauli za Ashura mara tu baada ya Fred kumfikishia taarifa za kwamba anafikiria kwenda zake Saud Arabia kwa ajili ya kutafuta kazi.
“Hizo stori tu.. ukiwasikiliza sana watu utakata tamaa, kwanza kuna muda huwa wanazusha zusha tu,” Fred alijibu.
“Fred Fred mama yako anakutegemeaa, acha ujinga,”Ashura akaongeza kwa msisitizo.
“Nisikilize Ashura mimi nilitegemea wewe ndio utakuwa mtu wa kwanza wa kunipa moyo kwa maneno ya matumaini lakini ndio unakuwa wakwanza kunipa maneno ya kunivunja moyo, kwanza hao ambao huwa wanateswa sijui na kutolewa mafigo ni wale wanaoenda kufanya kazi za ndani, mimi kwenye supamaketi hayo masuala ya kutolewa mafigo yatanikuta saa ngapi, halafu kule naenda kwa jamaa yangu mimi”Alisema Fred kwa uchungu huku akiwa anamuangalia Ashura.
Wawili hao muda huo walikuwa chumba kimoja na mmiliki wa chumba alikuwa ni Ashura, baada ya kusema maneno yale kwa uchungu Ashura alimsogelea Fred aliyekuwa kwenye kochi kisha akamkumbatia.
”Mimi sio k**a sitaki uende huko Mpenzi wangu, lakini nahofia usalama wako ndio maana nakuwa na wasi wasi k**a hivi, na yote hii kwa sababu nakupenda, sitaki uje kudhulika”Aliongea Ashura akiwa amekumbatia Fred huku nyuso zao zikiwa zinaangaliana..Mwisho wa tukio hilo lilikuwa ni siri ya kitanda.
Baada ya masaa kadhaa walipitiwa na usingizi hadi kufikia usiku kutokea asubuhi ambapo Fred aliingia kwenye chumba hicho.
“Mimi ngoja niondoke Ashura nafikiri tutaongea siku nyingine”alisema Fred huku akiwa anavaa suruali yake.
“Mmh! Kwahiyo tumefikia muafaka gasi sasa?” Ashura akaguna na kuachia swali lililomfanya Fred amtazame”
“Kuhusu nini?” Fred alijibu.
“Kuhusu hiyo safari yako”
“Wewe si umeniambia kwamba niende tu.”
“Ndio nimekwambia uende lakini hiyo pesa ya kwenda kuchukulia hiyo pasipoti sijui unaipata wapi na kile kigenge ndio ushakiuza,”Ashura alijibu na kumfanya Fred amtazame na asiwe na neno la kusema.
“Unaniangalia tu k**a nimewekwa makumbusho ya taifa usoni..wakati nimekuuliza swali,”Ashura akaongeza.
“Daah! Ashura mimi hapa nilipo hata akili yangu imenisaliti, natamani kuondoka hii nchi lakini kila nikifanya jihitada naona naenda kukwama tu, yaani k**a nimerogwa..”Fred akajibu na muda huo aliachana na zoezi lake la kuvaa suruali na akakaa tena kwenye kochi.
“Maskini wee! Sasa sikiliza mimi naweza kukukopesha kwa sababu naamini ukienda ukafanikiwa tutafanikiwa wote, lakini chonde chonde ukifika huko ukipata mshahara wako jambo la kwanza liwe ni kunirudishia pesa yangu, na sio sikupi hivi hivi tu, kuna sharti moja lazima ulitimize.”Aisha aliongea na kumfanya Fred atoe meno nje k**a Ngiri na kusikiliza kwa makini sharti atakalopewa.
“Kuna wanawake wana sifa za kuolewa na kuna wanawake wamezaliwa kwa ajili ya kuolewa, wewe ni miongoni mwa wale waliozaliwa kwa ajili ya kuolewa, nashukuru sana Ashura.’’Fred aliongea na kumsogelea Ashura.
“Unanishukuru wakati unatumia pesa yako, yaani hii sikupi nakukopesha utairudisha tu na k**a nilivyokwambia ni kwa masharti.”Ashura akamjibu Fred huku akitabasamu.
“Haya niambie ni sharti gani hilo?”Fred aliuliza.
“Lazima umwambie mama kwamba unataka kuondoka, tukubaliane mapema k**a si hivyo pesa umekosa”
Aliongea Ashura na kumkazia macho Fred ambaye aliinama chini kwa dakika kadhaa.
“sawa, nitafanya hivyo.”
Mrembo huyo aliamua kutoa kiasi cha laki tatu ambacho alikiweka kwa muda mrefu kila alipokuwa anapokea mshahara wake lakini kwa sababu aliamini mwanaume huyo ni wa maisha yake alikitoa bila ya kusita.

Baada ya kupata pesa hiyo kesho yake ambayo ilikuwa ni jumatatu asubuhi na mapema aliamkia ofisi za uhamiaji na kuanza kufuatilia mchakato wa kupata hati ya kusafiria.
Kwa kiasi hicho cha 200,000 sambamba na kiasi kidogo cha pesa alichokuwa nacho mchakato ulienda vizuri na baada ya kuwasilisha nyaraka zote aliambiwa kuwa aende wizara ya mambo ya ndani kwa ajili ya kuchukua Pasipoti yake baada ya wiki moja.
Siku ya ahadi ilifika lakini akaambiwa kuwa haikuwa tayari, hivyo angehitajika kusubiri kwa wiki nyingine.
Hakuwa na budi ikabidi avute subira hadi wiki iliyofuatia ambapo alifanikiwa kuipata na hakutaka kupoteza muda alimjulisha Mudi kwamba tayari alikuwa ameshafanikiwa kupata Pasipoti ambayo ndio ilikuwa nyenzo muhimu kwa ajili ya kuunganishiwa mchongo.
“Mzee baba sasa wewe sikilizia k**a wiki mbili hivi mimi naliseti jambo hapa, hadi muda huo kila kitu naamini kitakuwa tayari”Alisema Mudi mara tu baada ya Fred kumpa taarifa ya kwamba alishafanikiwa kuipata hadi ya kusafiria.
“Poa kaka mimi nipo nawewe na nakuaminia sana najua kila kitu kitaenda sawa kwa uwezo wa mungu”alijibu Fred ambaye alikuwa akiongea na Mudi kupitia mtandao wa kijamii wa Whatsapp kupitia kisimu janja chake kidogo cha Tecno H5.
Baada ya kuona mchakato unakuwa sawa Fred alitenga muda na kuketi na mama yake kumwambia juu ya adhma yake ya kutaka kutoka nje ya Tanzania kwa ajili ya kutafuta maisha.
“Mwanangu mimi nakuombea na nakupa Baraka zangu zote… maisha popote, wewe k**a unaenda kufanya kazi..kafanye kazi kweli usije tena ukafanya ambayo hayajakupeleka huko,”zilikuwa ni kauli za mama Fred mara tu baada ya Mwanawe kumwambia mpango wake.
Fred alionekana kuwa mwenye mshangao kwa sababu hakutarajia mama yake angepokea suala lile kirahisi vile, lakini hakutana kuonyesha hali yoyote kwenye uso wake.
“Mama mimi naenda kupambana kuiondoa hii hali ya umaskini, mimi inaniumiza sana kila nikiangalia maisha ambayo tunaishi, naamini nitarudi na mafanikio makubwa.”
Siku zilikatika na baada ya kutuma baadhi ya nyaraka ambazo Mudi alikuwa akimwambia atume kila baada ya siku kadhaa..hatimaye jioni ya Jumapili ya mwaka 2015, Mudi alimtumia ujumbe Fred kwamba kila kitu kilikuwa tayari na wiki ambayo ingefuatia angetumia makaratasi kwa ajili ya kuanza kufuatilia Visa kabla hajatumiwa tiketi ya ndege na kuanza safari.
Ilikuwa ni siku ya furaha sana kwa Fred baada ya kupokea barua hiyo na katika kipindi hicho kifupi kwa sababu hakuwa na kitega uchumi chochote ilimalizimu kufanya kazi za kiwandani k**a kibarua ili kuhakikisha mkono unaenda kinywani.
Wiki iliyofuatia makaratasi yalitumwa na akaanza mchakato wa kufuatilia Visa na baada ya wiki kadhaa alijulishwa kuwa Visa yake ilikuwa tayari na baada ya hapo siku tatu mbele alitumiwa tiketi ya ndege tayari kwa ajili ya kuianza safari.
“Fred usiwe na wasi wasi, najua hali ya mama ipoje mimi nitakakuwa natoa kila nitakachopata kuhakikisha yeye na ndugu zako wengine wanakula na mahitaji mengine hadi wewe utakapoanza kuwatumia pesa”
Yalikuwa ni maneno ya Ashura wakati wawili hao wapo uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere sambamba na familia ya Fred wakiwa wanamsindikiza jamaa huyo kwenye safari yake ya matumaini.
“Nashukuru Ashura, mimi sina chakukulipa kwa upendo wako huu, nakuahidi sitokuja kukuona wanini mbele ya macho yangu, nakupenda sana.”alisema Fred kisha akamkumbia Ashura wakiwa bado wapo nje ya uwanja huo.
“Mwanangu mimi nimekupa Baraka zote wewe nenda kapambane na naamini mungu atakusimamia,”Mama Fred naye alitoa salamu zake za mwisho kwa mwanawe kabla hajaondoka.
Baada kuagana Fred alienda sehemu ya ukaguzi kisha akapewa Boarding Pass na akapita tena sehemu nyengine ya kukaguliwa kabla hajapanda juu kabisa kwa ajili ya kusubiria muda wa kuingia kwenye ndege na kuanza safari.
Alikuwa akitumia shirika la ndege la Fly Emirates na baada ya dakika kadhaa aliingia kwenye ndege na safari ya kuelekea mji wa Riyadh huko Saud Arabia ikaanza.
Kwenye mji huo ndiko alipokuwa anaenda kufanya kazi, lakini ndege hiyo ilitua kwanza Dubai na kukaa kwa lisaa limoja kisha ndio ikaanza tena safari ya kuelekea Saud Arabia.
Ndege aina ya boeing 787 ilikanyaga ardhi ya Saudia kiasi cha saa 4:00 usiku na baada ya kutua walichukuliwa na basi ambalo lilitembea kwa dakika 20 hadi kufikia sehemu ambayo walishushwa na kuingia rasmi sehemu za kukaguliwa kabla ya kuruhusiwa kuingia rasmi nchini humo.
Wakati anatoka Tanzania alikuwa akiwasiliana na Mudi ambaye alimwambia kuwa ilibidi afikie kwake, kisha baada ya siku kadhaa ndio angempeleka kwa waajiri wake ambao wangempa nyumba ya kuishi muda wote atakaokuwa anafanya kazi.
Kazi ambayo aliambiwa kuwa angeenda kufanya ilikuwa ni kuwa mpishi kwenye mgahawa mmoja wapo Mjini Riyadh.
Hivyo baada ya kutua ikabidi aunganishe WIFI kwenye simu yake na kuanza kuwasiliana na Mudi kumjulisha kuwa tayari alikuwa ameshafika.
Fred alipita kwenye sehemu kadhaa za ukaguzi ikiwa pamoja na dawati la uhamiaji kabla hajaruhusiwa kupita baada ya kuonekana kwamba alikuwa sawa.
Wakati anatoka nje ya kuelekea sehemu ambayo watu huwa wanasubiriwa simu yake ikakata moto(chaji), lakini hakujali sana kwa kuwa aliona kwamba angemkuta Mudi kwenye eneo ambalo watu wanaowasili wanapokelewa na wenyeji wao.

Baada ya kufika eneo hilo ambalo lilikuwa limesheni watu hakumuona Mudi, taratibu wasi wasi ukaanza kuutafuna moyo wake, asijue hata afanye nini.
“Daah! sasa itakuwaje?”Kimoyo moyo Fred alijuliza.
Baada ya kusimama kwa muda aliamua kuketi kwenye moja ya viti huku akiangalia huku na kule akiamini kwamba angemuona mwenyeji wake.
Masaa mawili yakakatika, hiyo ilikuwa ni saa nane usiku na bado Mudi hakuwa ametokea.
Baada ya kuona muda unazidi kwenda akaamua kusimama na kumsogelea moja kati ya watu waliokuwepo karibu yake ili kuomba msaada wa simu awasiliane na Abdul.
“Excuse me! Can I borrow your phone, I want to contact my host, he didn’t show up until this time”aliuliza Fred kumwambia mama mmoja wa kiarabu aliyekuwa amesimama hatua kadhaa kutoka yeye alipokaa akimtaka kumuazima simu yake kwa kuwa mtu ambaye alitakiwa kuja kumpokea hakuwa ametokea hadi muda huo.
Lakini yule mama aliishia kumuangalia na asimjibu chochote.
Fred ilibidi afanye juhudi tena za kumuomba yule mama na safari hii aliamua kutumia ishara kwa kudhania kwamba huenda hakumuelewa.
Yule mama akasema”No no no” hiyo ni baada ya Fred kuweka vidole vyake sikioni kuashiria kwamba alikuwa na shida ya simu.
Wakati alipokuwa amekaa kwenye moja ya viti vya uwanjani hapo na likapita lisaa limoja.. Polisi waliokuwa wanalinda eneo hilo walimfuata na kumuuliza alikuwa akisubiria nini na alipowaambia kwamba mtu aliyetakiwa kumpokea hajafika waliachana naye.
Sasa tena baada ya kuona anaongea na yule mama na kumuonyesha onyesha ishara ya simu..walimfuata tena na kumuuliza kwamba alikuwa na shida gani na safari hiyo walionekana kuwa wakali kidogo.
Fred akaona inapoelekea anaweza akapelekwa sehemu ya mahojiano kwa kuonekana ni kibaka au tapeli ukizingatia rangi yake nyeusi.
Baada ya kufikiria kwa muda Fred alikata shauri na akaamua kuanza kujongea kutoka nje ya uwanja na safari hii hofu ikiwa imetanda sana moyoni mwake akiwa anahisi kuangusha machozi kwa kujiona kwamba ana mkosi.
“Balaa gani hili, mbona kila siku mimi, nikifanya hili linaibuka hili”alijisemea Fred kwa sauti huku macho yake yakiwa yamepambwa na maji maji yaliyoshiria huzuni iliyokuwa inamkabili kwa wakati huo.
Bahati mbaya Zaidi kwake hakuwa hata na kiasi chochote cha pesa cha kujikimu labda kununua chakula au maji.
Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Riyadh ni mkubwa sana hivyo hapo alipotoka ilimbidi kuanza kufunga safari nyingine hadi kufikia geti la kutoka nje kabisa.
Kila alipokuwa akizidi kufikiria jinsi alivyopambana.. ndio machozi yalizidi kumtoka na akashindwa hata kujizuia, akaamua kuangusha kilio kwa sauti.
Wakati akiwa anaendelea kulia huku anatembea kujaribu kutafuta geti la kutoka nje alisikia mtu anaongea nyuma yake.
“Mujomba vipi ndo nimefika naelekea nje?’ilikuwa ni sauti ya mwanaume aliyeongea Kiswahili kwa lafudhi ya kikenya.
Baada ya kusikia sauti hiyo Fred alipinduka kwa haraka kumuangalia mtu huyo aliyekuwa anaongea. Alikutana na mwanaume mwenye urefu wa kimo na kwa makadirio ya umri alifikisha kati ya miaka 30 hadi 35.
Fred alikata shauri na kuamua kusimama kumsubiri yule jamaa hadi amfikie kisha akamwambia:’’Kaka samahani, nina shida naomba unisaidie”
“Hee! Wewe unatokea wapi?”yule jamaa alionyesha kushangazwa baada ya Fred kuongea.
“Mimi naitwa Fred kaka natokea Tanzania,”alisema Fred kwa upole.
“Aaah, kumbe ndugu yangu kabisa, niambie, mimi natokea Kenya”yule jamaa aliongea huku akitabasamu.
Fred ikabidi amuelezee shida yake na jamaa hakuwa na hiyana alimpa simu ili atimize adhma yake.
NINI KITAENDELEA...?

RIWAYA HII INAPATIKANA FULL KWA SHILINGI 5000, AU KIPANDE KIMOJA KWA SHILINGI 500.

UNAWEZA KUIPATA HAPA FACEBOOK AMA WHATSAPP NICHEKI KUPITIA NAMBA 0687 058 966

Want your business to be the top-listed Gym/sports Facility in Dar es Salaam?

Click here to claim your Sponsored Listing.

Location

Website

Address


Dar Es Salaam