04/02/2021
FAIDA YA MAZOEZI YA KUKIMBIA KILA SIKU
Tatizo la unene linaongezeka kwa kasi katika jamii yetu, watu bado wamekuwa wakijisahau kufanya mazoezi ya miili yao licha ya kupata ushauri wa afya magazetini na sehemu nyingine mbalimbali wanapotoa huduma za afya.
Elimu ya lishe bora pamoja na ile ya kuishi vizuri kwa afya bora ni elimu muhimu sana kwa kila mtu kufahamu. Ukiwa na maarifa ya namna ya kula vizuri na kufanya mazoezi kwa afya, bila shaka utakuwa na upeo mkubwa wa kujua na kuelewa ni jinsi gani chakula na mazoezi vilivyo muhimu kwa maendeleo mazuri ya mwili wako na afya kwa ujumla.
Kuna sababu nyingi za mtu kutofanya mazoezi inaweza kuwa ni maradhi aliyonayo, kutoweka kipaumbele kufanya mazoezi ya mwili, ukosefu wa maarifa nakadhalika lakini swali muhimu la kujiuliza wewe mwenyewe hapa ni, je! Una sababu yeyote ya msingi ya wewe kutofanya mazoezi? Sababu nzuri ya wewe kutofanya mazoezi inaweza kuwa ni huna muda lakini ni jambo la busara kufikiri je! ni kweli unakosa angalau dakika 30 kwa siku kukimbia na kupata muda mwingi wa kutosha wa kulimbikiza mafuta mwilini yanayochangia uzito na unene wa mwili?
Zoezi la kukimbia lina manufaa mengi, hizi hapa ni baadhi ya faida;
1. Hurefusha Maisha.
Uchunguzi wa kisayansi umethibitisha kuwa kukimbia angalau kwa saa chache kwa wiki sio tu kutakufanya uwe mchangamfu na kuongeza utendaji wako wa kazi bali pia huongeza miaka ya kuishi.
2. Huimarisha Moyo na Mapafu.
Kwa mtu wa kawaida mwili hutumia oksijeni mara 10 zaidi wakati wa kufanya zoezi rahisi la kukimbia ukilinganisha na akiwa amekaa. Mtu anapofanya zoezi la kupasha mwili kwa muda huimarisha mfumo wa moyo wa usukumaji damu hivyo moyo na mapafu pia hufanya kazi zake kwa ufanisi.
3. Huboresha Utendaji kazi wa Ubongo na Kuongeza Uwezo wako wa Kufikiri.
Ikiwa inaaminika mazoezi ni afya, licha ya kuwa mazoezi yana manufaa mengi kiafya pia inaaminika mazoezi ya kukimbia husababisha ubongo kuzalisha homorne iitwayo ‘’endorphin’’ ambayo kemikali hii huibua hisia za furaha na kumfanya mtu awe katika hali ya kuwa na raha na mwenye mawazo chanya.
Sio tu kwamba mazoezi haya yatakufanya ujihisi katika hali ya furaha kwa muda bali yatakufanya pia uongeze ujasiri wako wa kujiamini na kujikubali mwenyewe hivyo pia utapunguza msongo wa mawazo na matatizo mengine yanayosababishwa na kuchoka kwa ubongo.
4. Hupunguza Uzito wa Mwili na Mafuta Mwilini.
Sote tunafahamu unapofanya mazoezi, baada ya muda utajisikia kuchoka, kutokwa na jasho, kuhema sana nakadhalika. Haya yote ni matokeo baada ya kufanya zoezi la kukimbia, unapofanya maozezi unachoma calories mwilini na hatimaye kupunguza mafuta.
Ikiwa utakuwa unafanya mazoezi ya kukimbia ipasavyo na kwa malengo ni rahisi kwako kuona mabadiliko ya mwili wako baada ya wiki chache. K**a wewe ni mnene na una uzito mkubwa wa mwili huu ndio wakati wako wa kuanza kufanya mazoezi ya kukimbia.
ZINGATIA HILI
Kumbuka kumuona daktari kwanza kwa vipimo na ushauri ili kufahamu afya yako kabla ya kuanza mazoezi ya aina yoyote.
06/06/2020
16/08/2016
16/08/2016
16/08/2016